Wakaazi wa eneo la Ahero wamehimizwa kukaa macho ili kujiepusha na walaghai wanaoitisha pesa wakidai ni maejenti wa kampuni ya kusambaza stima nchini Kenya Power.
Taarifa kutoka eneo hilo zinaarifu kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijitokeza kudai kuwa maejenti wa kampuni hiyo ya umeme punde tu baada ya mwakilishi wa wadi eneo hilo Maurice Aloo kuwafahamisha wakaazi kuwa wataunganishiwa umeme kwa gharama nafuu.
Aloo amewahimiza wakazi wote wa Ahero kuhakikishia kuwa malipo ya kuunganishiwa umeme yanafanyiwa tu kwa afisi za Kenya Power zilizoko Kisumu.
Ameongeza kuwa mshukiwa mmoja tayari ametiwa nguvuni na kwamba sheria lazima itachukua mkondo wake kwa wahusika matapeli.
''Ni jukumu la walinda usalama kuona kuwa watu wa aina hii wanatiwa nguvuni na tayari aliyekamatwa ni tapeli ambaye ni mmoja wa wakazi eneo hili,'' akasema Aloo.