Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika Kaunti ya Nakuru Peter Nderitu amesema mikakati ya kuhakikisha viongozi watenda kazi ndio wanaongoza serikali inaanzia na kuwa na kura mkononi.
Akiongea siku ya Jumamosi katika eneo la Wanyororo, Bahati, Nderitu alisema watu wanasusia kujiandikisha kupiga kura kutokana na hofu ambayo imewaingia wakazi kufuatia madai mengi ya ufisadi.
Alisema watashirikiana sako kwa bako na maafisa wa IEBC kuhakikisha watu wengi eneo lake hilo wanajiandikisha kama wapiga kura kwa kupeleka huduma hizo karibu nao.
Aliwataka wananchi pia kufahamu kwamba wao ndio wenye uwezo wa kuamua muwaniaji wa kiti chochote cha kisiasa, na hivyo kukosa kujiandikisha kupiga kura ni kufeli Kenya pakubwa.
“Kwa sasa hatufanyi siasa, lakini baada ya miezi 20 ijayo, utahitaji kadi yako ya kura ili kuuliza uliowachagua 2013 wamekufanyia nini. Kama tutakuwa tumekufeli, utasema kwa kura hiyo twende nyumbani, na kama tutakuwa tumefanya maendeleo, utasema pia kwa kura hiyo turudi afisini,” alisema Nderitu.
“Kiti hiki (cha mwakilishi wa wadi) mlichonipa kwa sasa kimevutia watu 20, mimi nahesabiwa kama wa ishirini na moja. Kwa hivyo utahitajika kama mpiga kura kutupiga msasa sisi sote,” aliongeza.
Nderitu, aliyekuwa akiongea na wakazi waliokongamana kusherehekea kufuzu kwa kijana Ben Mwaura kutoka chuo kikuu cha Presbyterian alikosomea udaktari, aliwataka wakenya kutokufa moyo wa kuwa na maisha bora, ambapo aliwahimiza wazazi kuwapa elimu wao kama uridhi wa kipekee, kwani hamna mashamba tena ya kuwagawia.
“Pia wasio kuwa na vitambulisho wafanye hima wazichukue,” akasema Nderitu.