Wakazi wa kijiji cha Matutu, Wadi la Gesima, wamelalamikia hali mbovu ya barabara katika eneo hilo.
Wakazi hao walimsihi mwakilishi wadi wa eneo hilo kupeleka mswada bungeni ili eneo hilo litengewe pesa zakufadhili ukarabati wa barabara.
Wakiongozwa na msemaji wao Nyakwana Orogo, wakazi hao walisema kuwa barabara za Karantini na Matutu, ziko katika hali mbaya hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara kubwa kwenye biashara zao.
Walimrai mwakilishi wa eneo hilo Ken Atuti, kuhakikisha kuwa pesa zakukarabati barabara hiyo zimepatikana.
"Tuna watoto wanaoenda shule kwa kutumia barabara hizi na kwa kweli kwa mara nyingi huwa vigumu kutumia barabara hizo, kwa kuwa zimejaa matope. Biashara zetu pia zimeathirika pakubwa na tunamwomba mwakilishi wetu apeleke mswada kwenye bunge la kaunti ya Nyamira ili eneo hili litengewe pesa zakukarabati barabara ambazo ziko katika hali mbaya,” alisema Orogo.
Simon Obiri, mkazi, alimwomba mwakilishi wa eneo hilo kuhakikisha kuwa vijana wa eneo hilo ambao hawana kazi wanapewa nafasi zakukarabati barabara hizo.
"Kuna idadi kubwa ya vijana katika eneo hili ambao wengi wao hawana kazi na ninamwomba mwakilishi wa eneo hili kuhakikisha vijana wananufaika kwa kupewa kazi ya kukarabati barabara hizi,” alisema Obiri.