Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi katika Kaunti ya Mombasa wamemtaka Gavana wa kaunti hiyo Hassan Joho Kuzingatia sheria kikamilifu atakapokuwa akizipa barabara majina ya watu ambao wametoa mchango wa kueleweka katika jamii.

Haya yamejiri baada ya bunge la Kaunti ya Mombasa kupitisha hoja inayompa nguvu gavana wa kaunti hiyo mamlaka ya kuzipa majina barabara za kaunti hiyo pamoja na majengo ya mji huo.

Hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na mwakilishi mteule katika bunge hilo Mohammed Hatimi siku ya Jumatano imempa gavana mamlaka ya kuyapa majengo na barabara majina ya watu ambao ni mashuhuri na pia walioleta mabadiliko ya kupongezwa katika taifa.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Bakari Chengo alisema kuwa hatua hiyo huenda ikawa ni kwa sababu ya kashfa aliyomiminiwa Gavana Joho baada ya kubadilisha jina la barabara ya Nyali na kuipa jina la mwanae kinara wa Cord Raila Odinga, mwendazake Fidel Odinga.

Achieng' Sibuor lalisema hatua hiyo ilikua nzuri, lakini akaongezea kuwa bunge ingehusisha maoni ya wenyeji kabla ya uamuzi huo kutolewa.

"Gavana anaweza akachagua jina lakini pia sisi tuhusishwe ili kusishuhudiwe malumbano tena," alisema Sibuor.

Omar Mwatseya alisema kuwa sheria inapaswa kufuata mkondo isije ikawa mamlaka hayo ni ya kutaja watu kiholela holela hata wale ambao hawafai kutajwa.