Wakazi Mombasa wamepongeza hatua ya kumchunguza tena aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru kama mhusika mkuu kwenye sakata ya ufisadi wa shilingi milioni 791 za shirika la NYS.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatano, wakaazi hao walisema kuwa uchunguzi huo unafaa kufanywa kwa kina ili kubaini wahusika halisi na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Halima Mahad, mkazi kutoka Buxton, alisema kuwa sharti waliohusika kukabiliwa kisheria ikizingatiwa walifuja fedha za umma.
Itakumbukwa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC ilitangaza kuwa imeanzisha upya uchunguzi katika sakata ya ufisadi ya shilingi milioni 791 za shirika la kitaifa la huduma kwa vijana NYS, baada ya kuibuka taarifa mpya katika hati ya kiapo inayomuhusisha aliyekuwa Waziri wa ugatuzi Ann Waiguru kama mhusika mkuu kwenye sakata hiyo.
Mkuu wa masiliano katika tume hiyo Karichi Marimba, alisema kuwa uamuzi wa kuchunguza upya faili ya kesi hiyo unatokana na taarifa zilizoibuka kutoka kwenye hati ya kiapo iliyowasilishwa na Josephine Irungu Kabira, mshukiwa mmoja katika kesi hiyo.
Katika hati hiyo ya kiapo iliyowasilishwa katika mahama kuu siku ya Jumatatu, Kabura aliapa kuwa Waiguru alihusika katika kashfa hiyo ya shilingi milioni 791.
Siku ya Jumatatu, mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko aliagiza Josephine Irungu Kabura na wengine kumi kufunguliwa mashtaka ya utumizi mbaya wa fedha za umma.