Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Meneja wa Kituo cha huduma kwa jamii (Huduma Centre) eneo la Mombasa, amesema serikali itaendeleza ugatuzi ili kufanikisha malengo ya wakazi wa mashinani.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Alex Murithi alisema kwamba kituo hicho kimesaidia kurahisisha shughuli za wakazi kwani kila kitengo cha serikali kimeidhinishwa katika kituo hicho.

Kulingana na Murithi, jumla ya wakazi 2,500 hupokea huduma hizo kila siku bila ya changamoto zozote.

Murithi alisema kwamba hatua ya kubuniwa kwa kituo hicho imechangia pakubwa kupunguza ufisadi katika idara za serikali humu nchini.

Aidha, alisema kwamba kituo hicho kinatoa huduma za kiserikali ikiwemo huduma za malipo ya uzeezi NSSF, huduma za hazina ya matibabu NHIF, huduma za wizara ya afya na huduma za Halmashuri ya utozaji ushuru nchini KRA ikiwemo huduma zingine za kiserikali.

“Tunawahimiza wakazi kutumia fursa hii kuzuru vituo hivi na kupata huduma zote za kiserikali kwa kuwa zile changamoto walikuwa wakipitia sasa zimepungua kabisa,” alisema Muriithi.

Murithi aliahidi kuzuru mashinani na kuihamasisha jamii kuhusu huduma za kituo hicho ili kufanikisha malengo ya ugatuzi yanayoshikizwa na serikali.