Wakazi wa Kaunti ya Mombasa wametakiwa kuwa waangalifu na kuvifunika visima vyao hususan wakati huu kunakoshuhudiwa mvua ili kuepukana na majanga.
Kulingana na Afisa mkuu wa Shirika la Maji na Ufanisi eneo la Pwani Bi Hamisa Zaja, mara nyingi visima vingi katikati mwa mji wa Mombasa huwa havifunikwi na kuchangia majanga ya watu kutumbukia katika visima hivyo wakati vimefurika maji.
Akiongea mjini Mombasa na wanahabari siku ya Jumatatu, Bi Zaja alisema kwamba ni lazima wakazi wawe waangalifu na kuvifunika visima hivyo ili kuepukana na majanga yanayotokana na visima kujaa maji wakati wa mvua.
"Visima vilivyochimbwa lazima vifunikwe ili kuzuia kushuhudiwa kwa majanga kwani wakati huu wa mvua, visima hivyo hujaa maji na ni rahisi kwa mtu kutumbukia kama kisima hakijazibwa,” alisema Zaja.
Aliwahimiza wamiliki wa majumba makubwa kukarabati mitaro ya kupitisha maja taka ili kuzuia maji hayo kuchanganyika na maji ya visima na kusababisha maradhi ya kiafya.
Hata hivyo, amependekeza washusika kutoka idara za mazingira kuzuru maeneo ya mashinani na kuchunguza visami hivyo ili kuhakikisha viefunikwa kama njia moja ya kuboresha mazingira bora kwa wakazi wa kaunti hiyo.