Wakazi jijini Mombasa wametakiwa kushirikiana katika kuboresha hali ya usafi ili kuwa na mazingira bora.
Akizungumza siku ya Jumanne, kaimu waziri wa maji na mazingira kaunti ya Mombasa Lewa Tendai alisema kuwa hatua hiyo itawakinga wakazi kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama kipindupindu.
Aidha, aliongeza kuwa wizara yake inajitahidi pakubwa katika kuboresha mazingira jijini kama njia moja ya kuhakikisha kuwa jamii ina afya bora.
Vilevile, aliahidi kushirikiana na wizara ya afya katika kuboresha hali ya usafi na kutibu magonjwa yanayotokana na uchafu.
Wakati huo huo, Tendai alisema kuwa kwa sasa serikali ya kaunti imeongeza magari ya kubebea taka kutoka 42 hadi 63, ili kuhakikisha shughuli za usafi zinaboreshwa.
Aidha, alisema kuwa idadi ya wahudumu wanaosafisha maeneo ya kumwaga taka vile vile imeongezwa.
Lendai alitoa onyo kwa watu watakaopatikana wakitupa taka kiholela kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kutoa faini ya shilingi 100,000 ama kutumikia kifungo cha miezi sita gerezani.