Wakazi wa Nakuru wanaotumia maji kutoka visima wameombwa kuchemsha maji hayo kabla ya kuyatumia haswa msimu huu wa mvua.
Afisa mkuu wa afya ya umma katika Kaunti ya Nakuru Samwel King'ori alisema kuwa visima vingi vimeingiwa na maji taka hali aliyosema inahatarisha maisha na afya ya wakazi wanaotumia maji hayo.
Akiongea siku ya Ijumaa alipotoa dawa za kutibu maji kwa wakazi wa mitaa ya Bondeni na Flamingo, King’ori aliwataka wakazi kuhakikisha kuwa maji wanayoteka kutoka kwa visima hivyo yamechemshwa na baadaye kutiwa dawa kabla ya kutumiwa.
Alisema kuwa mvua inayonyesha inabeba uchafu wa kila aina ya kuuteremsha visimani jambo ambalo alisema linachafua maji hayo.
“Mvua inaponyesha hubeba maji taka na uchafu mwingine na kuupeleka visimani na hii imesababisha maji ya visima kuchanganyika na maji taka na hivyo kuleta hatari kwa watumizi wa maji hayo,” alisema King’ori.
“Ni lazima wanaoteka maji ya visima kutibu maji hayo na kuyachemsha kabla ya kuyatumia nyumbani ili kuepusha hatari ya kuambukizwa magonjwa yanayoletwa na utumizi wa maji chafu,” alisema King’ori.
Aidha, afisa huyo aliwataka wenye visima kuhakikisha kuwa visima vyao vimefunikwa vizuri ili kupunguza uchafu unaoingia humo ndani.