Wakazi pamoja na wafanyibiashara katika eneo la Tala walifanya maandamano siku ya Alhamisi kulalamikia unyanyasaji kutoka kwa maafisi wa polisi.
Wakazi hao, wakiongozwa na mwenyekiti wa soko la Tala Anna Kyalo waliandamana kutoka sokoni hadi katika Kituo cha polisi cha Tala huku wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa majina ya maaskari wanaotaka waondolewe.
Mwenyekiti huyo alidai kuwa askari hao hufika katika sehemu za kazi kama vile vilabu na mahoteli, na kuagiza vyakula na vinywaji na kukosa kulipa.
Haya yanajiri siku tatu baada ya mwanamke mmoja, mhudumu wa kilabu, kupigwa na kuumizwa na askari wa polisi alipomwagiza kulipa pombe aliyoinywa.
Mhudumu huyo, Maryann Mwelu, alidai kuwa askari huyo alimlazimisha kunywa mabaki ya pombe yaliyochanganywa na maji, baada ya kumtishia maisha yake.
Wakazi hao aidha walilalamikia utendakazi wa askari wa eneo hilo.
Naibu kamishna wa Matungulu Patrick Mwangi alisema kuwa swala hilo litashungulikiwa.