Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa eneo la Rahma, kaunti ya Garissa, wametakiwa kuwa waangalifu na kuwatahadhari wanao dhidi ya kutumia mitandao za kijamii.

Huu ndio wito wa kutoka kwa wazee wa eneo hilo baada ya vijana wawili kutusiana, kuzozana na kisha kupigana na kupelekea mmoja wao kulazwa hospitalini baada ya kupata majeraha mabaya mwilini.

Kiongozi wa wazee hao, Hassan Hamdi, akiongea katika mkutano uliofanyika siku ya Jumatano jioni katika eneo hilo, alisema kuwa wamechoshwa na tabia ya kuona vijana wa eneo hilo wakiumizana kufuatia matusi na mzozo unaotokana na matumizi ya mtandao wa kijamii.

“Nataka vijana wa eneo hili kuwa na nidhamu na heshima ili walete mabadiliko katika eneo hili,” alisema Hamdi.

Kiongozi huyo aliwataka wazazi wote wa eneo hilo kuwapa nasaha na ushauri wanao unaozingatia ubaya wa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuwa hilo litasaidia pakubwa katika kupunguza visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa vijana wa Rahma.

“Ni matumaini yangu kuwa maelekezi ya wazazi kwa watoto wao itasaidia vijana wetu kuwa na adabu, heshima na nidhamu,” alisema Hamdi.

Mwishowe, walipanga kumchangishia pesa kijana yule aliyelazwa hospitalini ili wampelekee hela kidogo ya matumizi wakati huo ambapo anapokea matibabu.