Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku sherehe ya kusherekea siku kuu ya Jamuhuri zikiadhimishwa hiyo jana, siku ya Jumamosi kote nchini,  baadhi ya wakazi wa kaunti ya Kisii hawakuona umuhimu wa sherehe hizo kamwe.

Baadhi wa wakazi ambao waliona umuhimu wa siku hii walifika katika uwanja wa michezo wa Gusii kusherekea pamoja na viongozi wa serikali, huku wale ambao hawakuona haja ya siku hii wakiendelea na shughuli zao za biashara kama kawaida kwa kutafuta lishe kwa wanao.

Wakizungumza na mwandishi huyu mjini Kisii baada ya shuguli ya kusherekea siku hiyo kukamilika, Daniel Mose, ambaye ni mfanyibiashara wa kuuza viatu mjini Kisii na ambaye alikuwa anaendelea na shuguli zake za uuzaji alisema kuwa haoni haja ya siku hiyo ya Jamuhuri, jambo ambalo lilimfanya kuendelea na shughuli zake za biashara.

“Viongozi na matajiri waliona siku hii kuwa ya umuhimu kwao maana wako nazo (pesa), na kwa upande wangu ni lazima ningeendelea na biashara zangu ili nijipatie riziki kwa watoto wangu alisema,” alisema Mose.

Kwa upande wa wachuuzi waliokuwa wakiuza bidhaa zao mbalimbali kando kando mwa mwa barabara za mji wa Kisii, wengi walikiri kuwa serikali ya kitaifa na zile za kaunti zinastahili kuinua maisha ya kila mwananchi ili kila mmoja aweze kufurahia matunda ya uhuru na kuadhimisha siku kuu na sio kusherekea wakiwasahau wengine.

“Serikali zinastahili kusambaza rasilimali katika sehemu mbalimbali haswa za mashinani ili kila mmoja aweze kufurahia matunda ya uhuru wa kitaifa na sio sherehe kila wakati zisizo na umuhimu kwa watu wa tabaka la chini,” alisema Douglas Kombo mfanyibiashara.