Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wiki moja tu baada ya mke wa Rais Magret Kenyatta kuipokeza serikali ya Kaunti ya Nyamira kliniki tamba ili kuwawezesha wakazi kupata huduma za matibabu kwa haraka, wakazi wa eneo la Kebirigo wamepata sababu yakutabasamu baada ya gari la kliniki hiyo tamba kukita kambi katika eneo hilo kwa siku mbili.

Kulingana na mkazi mmoja wa eneo hilo aliyepata huduma hizo siku ya Jumapili kwa jina Gladys Boyani, hatua hiyo ilikua ya manufaa sana kwa wenyeji wa eneo hilo.

"Kwa kweli ni furaha kwa maana nilipata huduma za haraka kwa gari hili la kliniki tamba na nikajifungua mvulana kwa salama, hali ambayo haijakuwa kawaida kwa wakazi wengi wa maeneo haya kwa maana kina mama wamekuwa wakilazimika kuzuru zahanati na hospitali ili kujifungua," alisema Boyani. 

Boyani aliongeza kwa kushukru shirika lisilo la serikali la Wemyss Foundation kwa ushirikiano na Kenyatta kwa kuweka maslahi ya kina mama mbele kutokana na kupokeza kaunti mbalimbali kliniki tamba.

"Ningependa kumshukru Mama taifa kwa ushirikiano na shirika la Wemyss kwa kutupokeza kliniki tamba kwa kuwa hakika badala ya kuzuru hospitali kuu ya Nyamira ili kujifungua, kina mama kama mimi wanaweza pata huduma za gari hili na kujifungua salama, hatua ambayo itaimarisha zaidi huduma za afya nchini," alisema Boyani. 

Awali katibu wa afya katika serikali ya Kaunti ya Nyamira Douglas Bosire alikuwa amenukuliwa akisema kuwa kliniki hiyo itawahudumia wakazi wa kaunti ndogo tano za Nyamira zikiwemo Nyamira kaskazini, Nyamira kusini, Masaba, Borabu na Manga bila ubaguzi.