Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Manga walifanya maandamano siku ya jumatatu kulalamikia ongezeko la visa vya uajiri wa watoto katika maeneo mengi ya Gusii. 

Wakiongozwa na mwanaharakati wa haki zakibinadamu kutoka shirika la Mars Group Philip Mong'are, wakazi hao waliwaomba maafisa wa polisi kufanya misururu ya misako ili kuwaokoa baadhi ya watoto ambao wangali wameajiriwa kufanya kazi kwenye boma za baadhi ya wakazi wa eneo hilo. 

"Tumeungana pamoja kuandamana kulalamikia uajiri wa watoto wanaostahili kwenda shule na maafisa wa polisi wanastahili kufanya misako mikali ili kuwaokoa watoto kutokana na uajiri huo wa mapema. Yeyote atakaye patikana akihusika anastahili kutiwa mbaroni na kushtakiwa mahakamani," alisema Mong'are.

Aidha alimsihi kamishna wa kaunti hiyo Josphine Onung'a kuhakikisha kuwa afisi yake inaimarisha kampeni dhidi ya uajiri wa watoto, akihoji kuwa umaskini huchangia sana kwa watoto wadogo kuajiriwa kwenye boma za watu kabla yakuhitimu umri. 

"Uajiri wa watoto ni kosa kisheria. Hata hivyo, serikali haijaimarisha mikakati yakuhakikisha kuwa visa vya uajiri wa watoto vimethibitiwa na tayari tumemwandikia barua kamishna Onung'a na tunatarajia kuwa atatusaidia pakubwa kupunguza visa hivi," alihoji Mong'are. 

Haya yamejiri baada ya maafisa wa shirika linalo jishughulisha na uokozi wa watoto kutokana na uajiri wa mapema kule Nyansiongo kuwaokoa watoto wanne kutoka boma ambazo walikuwa wakifanya kazi ngumu bila malipo.