Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi kutoka katika eneo la Mtongwe wamemshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuzuru eneo la Pwani na kuangazia masaibu yanayowakumba na matatizo ya mara kwa mara ya feri katika kivuko cha Likoni Kaunti ya Mombasa.

Wamemtaka kushnikiza na kutumia mamlaka yake ili watu kutoka eneo la Mtongwe wapate feri yao ya kuhudumu kama zamani.

Wakiongea siku ya Jumanne na mwandishi huyu katika eneo la KD huko Mtongwe kupitia kwa mzee Ramadhan Saro, walisema kuwa imekuwa shida kwao kutekeleza majukumu yao ikizingatiwa kuwa kila siku lazima watumie kati ya shilingi sabini kama nauli kutoka na kuelekea eneo la Likoni ili kuvuka kuingia kisiwani kwenye shughuli zao za kutafuta riziki hali ambayo wanasema inawakandamiza kuinuka kiuchumi huku wakidai kuwa wengi wao ni wa kazi za vibarua.

Mzee Saro alitoa mwito kwa Rais kuwajali wakazi wa eneo hilo ambao wameteseka kwa mwaka wa tano tangu feri ya eneo la Mtongwe kuondolewa kwenye kivuko cha Mtongwe kwa sababu ambazo hawajahi kujua ni zipi.

Alisema kuwa shirika la feri limekuwa na mtindo wa kutosikiliza maoni ya wakazi na watumiaji wengi wa kivuko hicho na hufanya mambo yao kwa njia za kiimla ambapo ni hali hiyo imechangia kuwa kwa masaibu ya sasa kwenye feri hizo.

Alipendekeza kurejeshwa feri ya Mtongwe ili kupunguza watu wanaotumia feri na kwa kuchukua hatua kama hiyo kusaidia pakubwa misongamano ya watu ambao wanabanana kila asubuhi na jioni kuenda na kurudi manyumbani.

Rais Uhuru Kenyatta alikuwa kwenye kivuko cha Likoni siku ya Jumatatu ambapo alijionea yale yanayotendeka kwenye feri na kuahidi kuwa serikali itafanya kila inaloweza kuleta suluhu la kudumu kwenye kivuko hicho.