Wakazi wa kaunti ya Kisii wamehimizwa kutotoa hongo katika afisi yoyote ya serikali ili kuhudumiwa.
Wito huo umetolewa baada ya madai kubainika kuwa kuna baadhi ya wafanyikazi katika ofisi za serikali ambao huitisha hongo ili kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungmza siku ya Alhamisi mjini Kisii, Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi aliomba wananchi wa kaunti hiyo kutotoa hongo yoyote katika ofisi za serikali ili kuhudumiwa kwani ofisi hizo zimefunguliwa ili kuwahudumia wananchi.
“Naomba kila mtu asikie yale ninayosema hapa, mhudumu yeyote wa serikali akikuhitisha hongo ili akuhudumie, naomba upige ripoti kwa ofisi husika ambayo ni polisi ili afanyiwe uchunguzi wa kipekee na hatua kuchukuliwa hatua papo hapo,” alisema Maangi
“Ofisi za serikali zililetwa ili kutoa huduma bila malipo na kila mtu yuko na kibali cha kuhudumiwa bila hongo,” aliongeza.
Maangi aidha aliomba kila mwananchi na watumishi wengine wa serikali kushirikaiana pamoja kupambana na visa vya ufisadi katika kaunti ya Kisii .
Tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC ilifika katika Kaunti ya Kisii siku ya Alhamisi kuchunguza madai ya ufisadi katika serikali ya kaunti hiyo.