Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku msimu wa upanzi ukikaribia, wakulima katika eneo la Molo wanalalamikia kile walichokitaja kama bei ya juu ya mbegu na mbolea.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika eneo la Turi, wakulima hao walisema kuwa sasa wanahofia kwamba huenda hawatapata bidhaa hizi kwa muda ufaao, iwapo bei ya mbegu na mbolea itasalia kuwa ya juu.

"Mfuko wa kilo 50 wa mbolea unauzwa shilingi 3,200, huku ule wa kilo mbili ya mbegu ya mahindi ukiuzwa shilingi 360," alisema Michael Wanjau, mkulima wa eneo la Turi.

"Iwapo bei itasalia kuwa juu, huenda hatutapanda kwa muda ufaao. Itanibidi nipande mbegu kutoka kwa ghala langu bila mbolea," alisema Kamau Wang'ombe.

Wakulima hao sasa wanaiomba serikali kuingilia kati na kuwaletea mbolea ya bei ya chini.

"Mwaka uliopita, serikali ilituletea mbolea kwa bei ya chini na tunasihi mwaka huu pia wafanye vivyo hivyo,” alisema Mama Nyokabi.