Wakulima kutoka Uasin Gishu wamepokea magunia 600,000 ya mbolea kutoka kwa serikali.
Mbolea hiyo ni ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja ni ile ya DAP na mbolea nyinginezo za upanzi ambazo hazina kemikali.
Mbunge wa Moiben Silas Tiren alisema kufika kwa mbolea hiyo ni afueni kwa wakulima ambao kwa sasa wanajiandaa kwa msimu wa upanzi.
“Nashukuru serikali kwa kuleta mbolea ya kutosha msimu huu ambapo tumepokea mbolea tani 30,000 ambayo ni sawa na magunia 600,000 ya kilo 50. Mbolea hii imekuja wakati mzuri na itawawezesha wakulima kupanda mapema na kuhakikisha kuna usalama wa chakula,” alisema Tiren.
Tiren alisema kwamba wakulima sasa hawatakuwa na changamoto ya uhaba wa mbolea kama ilivyokuwa miaka ya awali.
Akihutubia wakulima ambao walifika katika ghala la Bodi ya nafaka na mazao nchini NCPB mjini Eldoret, Tiren aliitaka serikali kuhakikisha kuwa wakulima ambao waliwasilisha mahindi kwa bodi hiyo wamelipwa ili watumie pesa hizo kununua pembejeo za kilimo msimu huu wa upanzi.
“Ningependa kuambia Waziri wa fedha Henry Rotich ajaribu kadri ya uwezo wake ili kuona kwamba wakulima ambao waliwasilisha mahindi yao kwa NCPB wamepokea shilingi bilioni moja ambazo zilitolewa kwa wakulima ili wakulima lengwa wanufaike na fedha hizo,” alisema Tiren.
Bw Tiren aliitaka serikali kutengea sekta ya kilimo shilingi bilioni ishirini kutoka kwa bajeti ya kitaifa ili kuboresha uzalishaji wa chakula nchini.
Tiren alitoa changamoto kwa serikali kutekeleza mkataba wa Maputo kuhusu kilimo ili kuhakikishia Wakeya wana usalama wa chakula.