Share news tips with us here at Hivisasa

Walanguzi wa mihadarati katika kata ndogo ya Riamoni wameombwa kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kabla ya kutiwa mbaroni na kuwasilishwa kotini kujibu mashtaka.

Wakihutubu kwenye mkutano wa baraza siku ya Jumatatu naibu chifu wa Riooga Peter Orina na yule wa kata ndogo ya Riamoni Sambu Bosire, walisema kuwa wataanzisha msako mkali wa kuwatia mbaroni watu wanao nakisiwa kuendesha biashara hiyo kwenye kituo cha kibiashara cha Mosobeti.

"Ni jambo la aibu kuona kuwa baadhi ya vijana wadogo wamejihusisha kwenye uraibu wa dawa za kulevya katika maeneo mengi humu vijijini. Ninawaonya watu wanaojihusisha na uuzaji wa bangi kuwa sheria haitawasaza na wanastahili kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kabla yetu kuanzisha msako dhidi yao," alisema Sambu.

Kwa upande wake, naibu chifu wa Riooga Peter Orina, alisema kuwa wazee wa vijiji kwa ushirikiano na wadumishaji usalama vijijini watashirikishwa pakubwa kwenye msako huo wa walanguzi wa dawa za kulevya.

Aliwahimiza viongozi wa kisiasa kushirikiana nao ili kuhakikisha vijana wanasaidiwa kwa kupewa wosia wa kutojihusisha kwenye uraibu wa dawa za kulevya.

"Tuna ripoti kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi wanaotumia dawa za kulevya wamekuwa wakiuuziwa dawa hizo na walanguzi wa mihadarati katika eneo hili. Ninawasihi viongozi wa kisiasa kushirikiana nasi kuhakikisha kuwa hali hii inadhibitiwa, na ninatumai kuwa wazee wa vijiji wako tayari kushirikiana nasi kwenye msako huu mkali," alisema Orina.