Zaidi ya watu hamsini wanaoishi na ulemavu mjini Nakuru wamepokea zawadi za Krismasi huku wito wa upendo na kuwajali wasiyojiweza katika jamii ukisisitizwa.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika bustani ya Nyayo mjini Nakuru, mfanyibiashara Linah Towet, ambaye pia ni mfanyikazi wa kampuni ya umeme ya KPLC, alisema japokuwa watu kote duniani wanasherehekea siku kuu ya krisimasi, kuna baadhi ya watu ambao wasio na uwezo wa kusherehekea.
Aidha, Bi Towet alisema kuwa lengo la siku kuu ya krisimasi ni kushiriki kwa hali na mali na wale wasiyo na uwezo wa kupata kitu kutokana na changamoto mbalimbali.
Hatahivyo, Towet alisema kuwa hatua hiyo aliyoichukua kufurahikia na waliyo na ulemavu, haimaanishi kuwa analenga wadhifa wowote kisiasa, ila lengo lake ni kuona kuwa kila mtu ana sababu ya kutabasamu katika msimu huu.
Mwenyekiti wa kikundi cha Tegemeo, cha watu wanaoishi na ulemavu Richard Tirop, aliwaomba watu zaidi wenye heri njema katika Kaunti ya Nakuru na Kenya kwa jumla kuendelea kujitolea na kuwasaidia watu wasiojiweza.
Baadhi ya watu wanaoishi na ulemavu waliohudhuria hafla hiyo walitoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Nakuru kuweka mikakati kuhakikisha kwamba watu wanaoishi na ulemavu pia wanapata kukumbukwa.
Towet aliwapokeza unga wa ngano, mafuta ya kupikia, mchele, pamoja na vinywaji vya matunda.