Waliokuwa wafanyikazi kwenye mashamba ya aliyekuwa waziri wa ulinzi hayati Njenga Karume, wameitaka serikali kuwapa makao miaka michache baada ya serikali kununua mashamba hayo na kuwaacha bila makazi.
Maskuota hao ambao kwa sasa wanaishi katika mitaa duni mjini Molo wamelalama kwamba baada ya mashamba matatu ya Njenga Karume kununuliwa na serikali kwa kima cha shilingi milioni 69 kwa minajili ya kuwapa makao wahanga wa vita vya 1992, waliokuwa wafanyikazi wake kwa zaidi ya miaka 40 waliachwa bila kazi pamoja na mahali pa kuishi.
Utata kuhusiana na walionufaika na mashamba hayo ulizuka miaka kadhaa iliyopita baada ya watu wenye ushawishi mkubwa kunufaika na mashamba hayo badala ya IDPs na maskuota hao.
“Wafanyikazi hao wamesema Njenga alikuwa ametupa kipande kimoja cha ardhi kwa mustakabali watu lakini tulifurushwa kutoka kwa mashamba hayo na tumebaki tukihangaika,” alisema mmoja wao.
Kwa sasa wafanyikazi hao wameitaka tume ya kupambana na ufisadi pamoja na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kuchunguza sakata inayogubika umiliki wa mashamba hayo ili kufaidi wahanga wa vita vya 1992 pamoja na maskuota hao.