Wamiliki wa hoteli katika Kaunti ya Kisii wameshauriwa kuchukua nakala za vitambulisho vya wateja ambao wanahitaji kulala katika vyumba vyao.
Kamishna wa Kaunti ya Kisii alisema kuwa idadi kubwa ya wageni huwa hawawasilishi nakala zao za vitambulissho kwa wamiliki hao, jambo linalochangia katika kudorora kwa usalama.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, Chege Mwangi aliomba wamiliki hao kuchukua nakala za vitambulisho vya wateja wao, kama njia moja ya kuimarisha usalama.
“Ikiwa mnataka kuwa na usalama wa kutosha katika msimu huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya, sharti wamiliki wa hoteli waweze kuwatambua watu wanaokodisha vyumba hivyo. Wateja wanapswa kuwasilisha nakala za vitambulisho vyao kama njia moja ya kuwahakikishia wateja wengine usalama,” alisema Mwangi.
Aliongeza, “Hatua hiyo itawawezesha maafisa wa polisi kuwakamata wateja watakao husika na uhalifu.”
Wakati huo huo, Mwangi aliwahakikishia wakazi wa kaunti hiyo usalama wa kutosha wakati wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.
Aidha, Mwangi aliwaomba wakazi kuwa watulivu msimu huu wa krismasi na kuwaonya dhidi ya kuzua vurugu.