Share news tips with us here at Hivisasa

Chama cha wamiliki wa matatu mjini Mombasa kimeziomba kampuni za bima kuandaa tuzo maalum kila mwaka kwa madereva wanaozingatia sheria za trafiki barabarani.

Akiongea katika kongamano na wanahabari mjini humo siku ya Jumatatu, katibu mkuu wa chama hicho Salim Mbaraka alisema kuwa mbali na kuwaadhibu madereva wanaokiuka sheria, pia wale wanaozifuata wanafaa kutuzwa.

“Tunaomba kampuni za bima pia kuwatuza madereva wanaotii sheria za barabarani na kuhakikisha hakuna ajali inatokea, hiyo itatia motisha kwa madereva wengine pia,” Alisema Mbaraka.

Pia katibu huyo alichukua fursa hiyo kuhamasisha madereva kuwa waangalifu wakati huu wa sherehe ambapo watu wengi watakuwa wakisafiri na pia kuwasihi wananchi wanaotumia barabara kuwa makini.

Kauli yake inakuja siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhutubia wakenya siku ya Jamhuri akiwasihi wananchi kuwa waangalifu barabarani wakati huu wa sherehe za krismasi na mwaka mpya.