Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wanafunzi 200 wa shule ya sekondari ya Cheptoroi katika kaunti ya Nakuru jimbo ndogo la Njoro, Ijumaa walifanya maandamano ya amani kulalamikia kuhamishwa kwa mwalimu wao mkuu.

Wakiandamana na wazazi wao wanafunzi hao walitembea zaidi ya kilomita kumi hadi katika afisi za elimu mjini Njoro wakitaka kuzungumza na afisa wa elimu katika kaunti hiyo ndogo Irene Kithinji.

Bii Kithinji akiwahutubia, aliwataka kurejea shuleni na kuahidi kufanya ziara shuleni humo kujadili malalamishi yao.

Wakizungumza na wanahabari, wanafunzi hao walisema kwamba uhamisho wa mwalimu huyo wiki mbili zilizopita utakuwa na madhara makubwa ya kielimu kwao, kwani alikuwa akichangia pakubwa katika ufanisi wa kimasomo shuleni humo.

Na kama kutia chumvi kwenye kidonda, wanafunzi hao walisema kwamba usimamizi wa shule hiyo umekuwa ukiwatoza fedha nyingi za kugharamia maankuli, il hali chakula wanachopewa ni duni mno.

“Katika mkutano wa wazazi na waalimu Januari mwaka huu, tulikubaliana kwamba watoto wetu watakuwa wakipewa uji vikombe viwili kila siku. Kwa sasa wanaendelea kupewa uji kikombe kimoja tu,” alisema mzazi mmoja aliyejitambua kama Wanjiku Maina.

Mwandishi huyu hakufanikiwa kuzungumza na mwalimu huyo mkuu, kwani simu yake ilikuwa imezimwa.