Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshauri wa maswala ya uandishi habari nchini Vitalis Musebe, amesema huenda taifa hili likakwama kimaendeleo ikiwa matamshi ya chuki humu nchini hayatadhibitiwa haswa miongoni mwa wanasiasa.

Akizungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Ijumaa, Musebe alitoa wito kwa wanahabari kutokimya na badala yake kuwaangazia viongozi wanaoeneza chuki, ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watu wenye nia ya kusababisha vurugu Kenya.

Alitoa wito kwa wananchi pia kutoshabikia matamshi hayo na badala yake kukataa kugawanywa kikabila, kisiasa ama kidini.

“Matamshi hayo huenda yakatia hofu baadhi ya wawekezaji humu nchini na kupelekea wageni kususia kuzuru taifa hili,” alisema Musebe.

Vilevile, alisema kuwa matamshi hayo hudhoofisha umoja na utangamano wa kitaifa.

“Taasisi zilizotwikwa wajibu wa kuhakikisha kuna utangamano na uwiano nchini ikiwemo NCIC ni sharti zionyeshe makali yake kwa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa,” alisema Musebe.