Wananchi wote wameombwa kushirikiana pamoja kuhakikisha kuwa wanawake wengi wamechaguliwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika serikali ya Kenya.
Ombi hilo limetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya wanaume humiliki idadi nyingi ya viti katika nyadhifa za uongozi serikalini ikilinganishwa na idadi ya wanawake.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nyamira Alice Chae aliomba wananchi kushirikiana na wanawake kuhakikisha idadi ya viongozi kwa wanawake imeongezeka katika uongozi ujao katika kura za mwaka wa 2017.
Hata hivyo Chae alisema wanawake wanaweza kuyafanya yale ambayo wanaume wanayafanya na hakuna haja ya kususia kuwachagua wanapowania viti mbalimbli vya uongozi.
“Wananchi wenzangu haswa wale wa kupiga kura naomba kwa unyenyekevu muweze kushirikiana ili kuwachagua wanawake wengi katika nyadhifa mbalimabali za serikali,” alisema Alice Chae mwakilishi wa wanawake Nyamira.
“Wanawake nao wako na uwezo wa kuyatekeleza yale ambayo wanaume wanayafanya katika maendeleo na sekta zingine,” aliongeza Chae.
Wakati uo huo, mwakilishi Chae aliomba wanawake wengi kujitokeza kwa wingi kuviwania viti mbalimbali vya uongozi katika uchaguzi ujao kwani watachaguliwa kuwa viongozi kwani dalili zimeanza kuonyesha ishara za mapema.
“Naomba wanawake wengi kuchaguliwa kuwa viongozi na kuna haja yao kujitokeza kwa wingi ili kukabiliana na wanaume kwa debe ya kura,” aliongeza Chae.