Waziri wa usalama wa ndani meja mstaafu Joseph Nkasseiry amewaonya wanasiasa wanaochochea vijana kuwazoma wanasiasa wengine kwenye majukwaa akisema kuwa kamwe hawatolifumbia macho suala hilo.
Siku ya Jumamosi, Nkasseiry alidokeza kuwa idara ya usalama inawachunguza wanasiasa wanaotoa matamshi ya uchochezi na kuwataka kukoma tabia hiyo wakati huu ambapo joto la kisiasa linashuhudiwa.
Alieleza kuwa kila mkenya ana uhuru wa kuchagua kiongozi anayemtaka hivyo basi viongozi wa kisiasa hawana mamlaka ya kushurutisha kuchaguliwa kwa kiongozi.
Aidha, aliongeza kuwa vijana watakaopatikana wakiwazomea wanasiasa watakabiliwa kisheria.
Kauli hii ya Nkasseiry inajiri baada ya makundi ya vijana kuzomana mbele ya Rais Uhuru Kenyatta wakati wa uzinduzi wa mradi wa kitaifa wa Mwangaza Mitaani katika uwanja wa Makadara siku ya Ijumaa ambapo kundi moja lilionekana kumuunga mkono seneta wa Nairobi Mike Mbuvi na lingine la gavana wa Mombasa Hassan Joho.