Wanaume nchini wamehimizwa kujibidiisha kuwalinda wanawake dhidi ya dhulma za kijinsia.
Himizo hilo limetolewa na Peter Gichanga, mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Masculinity Kenya, lililo na lengo la kubadili dhana na mienendo inayohusishwa na dhulma za kijinsia, haswaa ile inayowadhuru pakubwa akina mama na wasichana.
Akizungumza kwenye hafla ya kutamatisha kampeni ya siku 16 ya kukabiliana na dhulma za kijinsia iliyofanyika siku ya Alhamisi kwenye bustani ya Nyayo jijini Nakuru, Gichanga alisema kuwa wanaume pia wanaweza kuathiriwa pakubwa kupitia kwa dhuluma zinazotendewa watoto wao wa kike, dada zao au pia mama zao.
“Baadhi ya wanaume husema kwamba ni lazima wanawake waadhibiwe. Unaposema hivyo, unasahau kwamba una mama, dada na pia mtoto wa kike. Haijalishi hadi pale ambapo ni mmoja wa yule ambaye ni jamaa yako anadhulumiwa. Wanaume wanapswa kufahamu kwamba mtoto wako wa kike au pia mama yako anaweza kuwa mwathiriwa wa dhulma za kijinsia,” alisema Gichanga.
Alitoa wito kwa wanaume kufahamu kwamba ni wajibu wao kupunguza na pia kukomesha dhulma za kijinsia.
Gichanga alisema wanaume wanaweza kufanya hivyo kupitia kwa njia mbalimbali kama vile kuripoti visa hivyo vya dhulma katika vituo vya polisi.
“Ningependa kuwapa changamoto wanaume kwamba kuanza leo, wanafaa kuhakikisha kuwa ni wajibu wao kukomesha dhulum za kijisnia. Unaweza kupiga simu kwa kituo cha polisi au kwa makundi ambayo hujihusisha na vita dhidi ya dhulma za kijinsia,” alisema Gichanga.
Gichanga alisema kuwa shirika lake linafanya kazi pamoja na makundi mbalimbali kama vile Movement of Men, kitengo cha kukabiliana na dhulma za kijinsia katika Hospital ya Nairobi, pamoja na serikali.