Share news tips with us here at Hivisasa

Wanawake wanaotumia kivuko cha feri cha Likoni wamelalamikia dhuluma za kimapenzi dhidi yao kutoka kwa baadhi ya wanaume ambao wanadai wamekuwa wakichukua nafasi yao wakti wa msongamano na kuwapapasa na kuwashika sehemu zao nyeti.

Wanawake hao wanasema kuwa mtindo huo umeendelea kwa muda mrefu, na wamekuwa wakilalamikia na kuwasilisha malilio yao kwenye mamlaka ya feri nchini, lakini hamna hatua muhimu imechukuliwa ili kuona dhuluma kama hizo zinapungua.

Wakiongozwa na mama Fatma Mwinyi katika kivuko hicho siku Alhamisi, walisema kuwa kina mama wanajipata katika hatari kubwa kunapotokea msongamano, na kuongeza kuwa vijana wengine wa kiume huendeleza tabia hiyo hata kwenye pantoni, kila wakati wanapokimbilia feri nyakati za asbuhi na majira ya jioni.

“Tunapatwa na dhuluma chungu nzima, baadhi ya wanaume hushikashika kwenye sehemu zetu nyeti nyakati mna msongamano, ikizingatiwa wakati huo tunakimbilia feri ili kufika kazini mapema, na hali hii imekuwa tangu nyuma hadi wakati huu bado ipo dhuluma,” alisema Mwinyi.

Japokuwa alilipongeza shirika hilo kwa kutenga banda la wanawake na lile la wanaume, lakini alishangaa ni kwa nini banda hilo hufungwa wakati fulani, na kunapokuwa na msongamano wanaume huingia kwenye banda lao na inakuwa vigumu kuwazuia kwa sababu ya mabanda hayo kukaribiana sana.

Waliliomba shirika hilo kutafuta mbinu mwafaka ya kuweka vizuizi wanaume kuingia kwenye banda lao.