Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya makundi ya kina mama kutoka wadi ya Manga wamejitokeza kumshtumu mwakilishi wa kina mama kwenye kaunti ya Nyamira Alice Chae kwa kuwatenga.

Wanawake hao walidai kuwa Chache amewatenga kwa kutowahusisha kwenye miradi ya maendeleo, na kutishia kutompigia kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Wakihutubu katika eneo la kibiashara la Manga siku ya Jumanne, wanawake hao wakiongozwa na msemaji wao Bi Grace Maisiba, walisema kuwa mwakilishi huyo wa kina mama kwenye bunge la kitaifa amekuwa akiwasaidia kina mama kutoka maeneo mengine ya wadi kuanzisha biashara bila ya kuyasaidia makundi ya kina mama kutoka eneo hilo.

"Tunafahamu kuwa Chae amekuwa akiyasaidia makundi mengine ya kina mama kutoka wadi zingine humu Nyamira kuanzisha biashara. Hatujui ni kwanini hajaonekana hapa Manga na kwa kweli huenda tusimpigie kura kwenye uchaguzi mkuu ujao," alisema Maisiba.

Wanawake hao aidha walidai kuwa juhudi zao za kutaka kumpata Chae ili kuwasilisha malalamishi na matakwa yao hazijafanikiwa, hali ambayo wanasema kuwa inadhihirisha uongozi mbaya kutoka kwa mwakilishi huyo wa kina mama.

"Kina mama ni watu muhimu sana katika kuimarisha maendelo miongoni mwa jamii, na tunashangazwa ni kwa nini mwakilishi Chae hataki kukutana nasi. Tungali tunahitaji kukutana naye ili kumweleza matatizo yetu," alisema Maisiba.