Huku zikisalia siku nne kabla kukamilika kwa zoezi la usajili wa wapiga kura kote nchini, sasa viongozi mbalimbali wamejitokeza kuwashinikiza wanawake kujisajili ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao.
Wakizungumza siku ya Alhamis mjini Mombasa, wanaharakati wa kutetea maslahi ya wanawake katika ukanda wa Pwani walisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa wanawake bado hawajajitokeza kwa usajili huo, licha ya muda wake kuelekea kukamilika.
Wakiongozwa na Mkurugenzi wa shirika la Wanawake na Maendeleo kanda ya Pwani CWID, Betty Sharon, wanaharakati hao walisema kuwa ili wanawake kufanikiwa katika maswala mbali mbali ya kimaendeleo, pamoja na kupiga vita dhulma za kijinsia na unyanyasaji, lazima washiriki katika uchaguzi na kuwateua viongozi watakaotetea maslahi yao.
Alisema kuwa iwapo wanawake wanataka swala la demokrasia kuangaziwa na kuimarishwa kwa usawa wa jinsia, basi lazima wajitokeze na kuungana pamoja katika uchaguzi mkuu kuwachagua viongozi waadilifu.
Alisema kuwa jukumu kubwa la wanaharakati hao ni kutetea maslahi ya wanawake na jamii kwa jumla, ili eneo la Pwani liweze kuasi visa vya dhulma za kijinsia.
“Tungependa kuwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi na kuungana na wenzao katika kujisajili kama wapiga kura kwani muda uliosalia ni mchache mno,” alisema Sharon.