Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku jamii ya Kiislam ulimwengu ikisherehekea vazi la hijab, wakaazi pamoja na waumini wa dini hiyo katika kaunti ya Mombasa wamewahiza kizazi kinachokua kulikumbatia vazi hilo la stara miongoni mwa jamii hiyo.

Wakiongea na mwandishi huyu katika jiji la Mombasa, waumini hao walisema kuwa sharti kila mtoto wa Kiislam hasa msichana, kuvaa vazi hilo kama njia moja ya kustiri mwili wake na pia kuonyesha heshima kwa wakubwa wake.

Sheikhe Salim Athman kutoka eneo la Liwatoni, aliwasihi watoto wa kike ambao wanathamini miili yao kuwajibikia utaratibu na hitaji kuu la dini zote ambazo zinawahimiza wanawake kujifunika mwili wao inavyopaswa.

Bwana Athman alisikitikia hali ya sasa ambako watoto wa kike wamekuwa na mtindo wa kuvaa vibaya, na wengine kuvaa nguo ambazo huwaonesha miili yao kwa hadhara.

Alisema kuwa mwili uwe wa mtoto wa kiume au kike sharti ufunikwe.

Mama Aisha Hamisi, ambaye ni mtoa ushauri nasaha kwa watoto wa kike kwenye dini ya Kiislam aliwataka wazazi kuwaongoza wanao kwa njia ya maadili na yenye mwelekeo wa dini.

Vazi la hijab ni maarufu miongoni mwa wanawake wa dini ya Kiislam na hutumiwa kufunika sehemu ya juu ya mwanamke hasa kusitiri kichwa na kipaji.