Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanawake wajawazito wameonywa dhidi ya kujifungua majumbani mwao na kuhimizwa kutembelea hospitali pindi tu muda wa kuzaa utakapofika ili kupata huduma bora.

Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya jumapili, muuguzi Asia Sulthana Sunkar, kutoka Saala Medical Clinic, alisema kuwa hatua hii itapunguza idadi ya vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga iwapo watapata huduma bora kutoka kwa daktari.

Asia alisisitiza kuwa wengi wa wanawake wajawazito hupoteza damu nyingi jambo linalopelekea wengi kufariki hasa wanapohudumiwa na wakunga wasio na ujuzi mitaani.

Aidha, aliongeza kuwa kupata huduma hospitalini kutapunguza kuenea kwa virusi vya ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto na hata kwa mkunga.

Vile vile aliongeza kuwa itakuwa vigumu kwa mama mjamzito kufanyiwa upasuaji iwapo atajifunguwa kwa usaidizi wa wakunga mitaani kinyume na hospitalini ambako kuna vifaa na huduma bora kutoka kwa wahudumu waliohitimu.

Kauli yake inajiri baada ya kina mama wengi kushuhudiwa kujifunguwa majumbani mwao hasa katika maeneo ya vitongojini.