Wito umetolewa kwa serikali ya kaunti Nakuru na ya kitaifa kuhakikisha kwamba inawapiga jeki wasanii chipukizi katika mitaa mbalimbali.
Ni kauli yake msanii chipukizi wa nyimbo za bongo Sharomat Deno kutoka mtaa wa Green view Nakuru.
Katika mahojiano ya kipekee, Deno ambaye kwa ushirikiano na wenzake wametoa vibao kadhaa ikiwemo 'Kiwewe' na 'mapenzi kweli' alisema kuwa kunavyo vipaji mashinani lakini havijatambuliwa.
"Kila mtaani kuna vipaji vinavyozidi kuchipuka lakini serikali bado kuvitambua na mie ni kurai tu vijana wasanii wapigwe jeki,"Deno alisema.
Wakati huo huo aliongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba ni wasanii tu waliobobea ambao wanatambuliwa humu nchini.
Kwa mujibu wake, hazina maalumu inafaa kubuniwa ili kukuza talanta mashinani.
Msanii huyu chipukizi wa Nakuru ambaye kwa sasa hujishughulisha na kinyozi mtaani Buruburu anasema kuwa:"La muhimu ni kupata riziki na vijana wasichague kazi."