Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Viongozi mjini Naivasha wameelezea wasi wasi dhidi ya kudorora kwa viwango vya elimu wilayani humo kwenye mtihani wa KCPE uliotangazwa wiki jana, haswa kwenye  shule za umma.

Sasa wanapendekeza kubuniwa kwa kamati maalum itakayochunguza kinachosababisha matokeo hayo kudorora mwaka baada ya mwingine.

Shule za kibinafsi za Little Friends, Lizar Junior, High Peak na Ridges View ni mojawapo wa zile zilizotoa wanafunzi bora pamoja na kuongoza kwenye mtihani huo wilayani Naivasha.

Kiongozi wa vijana kaunti ya Nakuru Charles Mburu, hata hivyo amechangamoto serikali kuwapa wanafunzi wanaotoka shule za kibinafsi nafasi sawa pamoja na wenzao wa shule za umma kujiunga na shule za upili.

“Kikatiba kila mtoto ana haki ya kusoma katika shule anayofaulu kuitwa, kwa hivyo serikali isiendeleze ubaguzi wakati wa kuchagua wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza,” alisema Mburu.

Mburu hata hivyo ameitaka serikali kuzipa uwezo zaidi shule za umma iwapo matokeo ya shule hizo yanatarajiwa kwenda sabamba na yale ya kibinafsi.

Kiongozi mmoja mjini Naivasha Antony Rebo kwa upande wake amesema kuwa ripoti kuhusu masomo ya wilaya hiyo iliyofanywa miaka miwili iliyopita inafaa kutolewa kwa umma.