Share news tips with us here at Hivisasa

Washukiwa wawili wa mauaji ya watu 12 huko Hindi Kibokoni watajua hatma yao tarehe Machi 23, 2016.

Hii ni baada ya wawili hao Swaleh Shebe na Joseph Kimani kukamilisha ushahidi wao dhidi ya madai yanayowakabili siku ya Jumatatu.

Wiki iliyopita jaji Martin Muya aliwapata na kesi ya kujibu kuhusiana na mauaji hayo ya mwaka 2014 huko Lamu.

Swalehe Shebe Auni alitokwa na machozi alipokuwa akielezea mahakama kuu jinsi alivyopigwa sehemu za siri na maafisa wa KDF.

Shebe aliambia mahakama kuu ya Mombasa kuwa alipelekwa msituni na wanajeshi na kupigwa sehemu zake za siri, huku akilazimishwa kukubali kuhusika na mauaji hayo.

Aliongeza kuwa wenzake wawili walipigwa risasi hadi kufariki na wanajeshi hao.

Aidha, alishikilia msimamo wake mbele ya jaji Martin Muya kuwa hakuhusika na mauaji hayo wala kuenda Somalia kujiunga na wanamgambo wa al-Shabaab kama inavyodaiwa na maafisa hao.

Aidha, aliambia mahakama kuwa hana chuki wa uhasama na jamii ya wakikuyu kama inavodaiwa ikizingaitiwa alioa bibi mkikuyu na kuzaa naye watoto wawili.

Wawili hao wanadaiwa kuhusika katika mauaji ya watu 12 huko Hindi, Kaunti ya Lamu, kati ya tarehe Julai 5 na 6 mwaka 2014.