Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Washukiwa watatu, akiwemo aliyekuwa afisa wa KWS, wanaotuhumiwa na ugaidi na kuwa na uhusiano na kundi la Al-shabab watasalia korokoroni kwa siku 30 kusubiri uchunguzi wa kesi yao kutamatika.

Hii ni baada ya afisa wa upelelezi Jackson Guyo kuwasilisha ombi katika mahakama ya Mombasa, mbele ya hakimu mkuu Diana Mochache, la kutaka watatu hao kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central ili kutoa nafasi kwa afisa huyo kukamilisha uchunguzi wake.

Washtakiwa hao Mohamed Hussein Warsame, Roble Kassim Abdi pamoja na Aden Abdullahi Abdi walikanusha kuwa na uhusiano na kundi la Alshabab wala kuhusika na ugaidi na kuiambia mahakama kuwa wao ni wawindaji haramu.

Mohamed Hussein Warsame, ambaye alikuwa afisa wa mbuga ya wanyama pori, aliiambia mahakama siku ya Alhamisi kuwa alifutwa kazi na idara ya wanyama pori mwaka 2008 na mpaka sasa bado hajalipwa pesa zake jambo linalomfanya kufanya kazi ya uwindaji haramu ili kujikimu kimaisha.

Watatu hao walitiwa mbaroni na maafisa wa usalama siku ya Jumatatu wakiwa na risasi 56, simu na vitambulisho sita katika hoteli moja ya kukodi eneo la Bondeni.

Kesi hiyo itatajwa mwezi Februari mwaka wa 2016.