Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Watoto wa mitaani maarufu kama chokoraa mjini Mombasa walipata fursa ya kujumuika pamoja katika sherehe zilizoandaliwa na makundi mbalimbali ya vijana yakushirikiana na kaunti hiyo.

Sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Makadara siku ya Jumatatu zilishuhudia idadi kubwa ya watoto hao ambao pia walipata fursa ya kuonyesha vipaji vyao pamoja na kupewa chakula cha bure.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharif Nasir pamoja na waziri wa vijana Kaunti ya Mombasa Mohamed Abas waliudhuria ambapo waliwapa watoto hao fursa ya kueleza matatizo wanayopitia na jinsi wataweza kusaidika.

Wakiongea baada ya kupewa fursa hiyo, watoto hao, wakiongozwa na mwakilishi wao Zakary Mutembei walieleza jinsi wamekuwa wakisumbuliwa na askari wa kaunti.

“Sisi shida yetu kubwa ni kusumbuliwa na askari wa kaunti, wakituona wanatukamata bila makosa na hiyo imefanya maisha yetu yamekuwa magumu,” alisema Mutembei.

Kwa upande wake waziri Abas alipokuwa akiongea na wanahabari alieleza umuhimu wa sherehe hizo.

“Hii ni fursa ambayo tumewapa watoto hawa watueleze changamoto zao kisha sisi kama kaunti tutajua vile tutawasaidia, na pia tumewapa sikukuu ya mapema kwa kuwaletea chakula,” alisema Abas.

Aidha, waziri huyo pia alisema kuwa serikali ya kaunti imetenga fedha maalum za vijana, na kuongeza kuwa wanaendelea na mikakati ya kuwasaidia watoto hao wa mitaani kutumia fedha hizo.