Share news tips with us here at Hivisasa

Watu watatu wameaga dunia kwenye ajali tofauti mjini Naivasha huku idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za kiholela vikiendelea kuongezeka.

Katika kisa cha kwanza, afisaa mmoja mkuu wa shirika la Kengen aliaga dunia mapema Ijumaa kwenye barabara ya Naivasha kuelekea Mai Mahiu, baada ya gari lake kugonga trela moja kutoka upande wa nyuma.

Mkaazi Joel Mwangi aliyeshuhudia ajali hiyo iliyotokea karibu na kijiji cha Chechnia, alisema ilifanyika mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Na katika kisa cha pili, watu wawili waliokuwa wakivuka barabara waligongwa na kuuawa na magari mawili tofauti walipokuwa wakivuka barabara ya Naivasha kuelekea Nairobi.

Mtu wa kwanza aligongwa karibu na eneo la Karai huku wa pili akigongwa karibu na kituo cha kufanyia biashara cha KCC.

Miili yote mitatu ilichukuliwa na maafisa wa polisi na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.