Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wawekezaji katika viwanda vya mafuta na biashara nyinginezo katika Kaunti ya Mombasa wamehimizwa kuwa na vifaa maalum vya kudhibiti majanga kama vile moto wakati yanaposhihudiwa.

Kulingana na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa Maxwell Masai, viwanda vingi katika kaunti hiyo bado havijanunua vifaa hivyo maalum vya kuzima moto na hivyo hushindwa kudhibiti majanga hayo, huku akisema kuwa kuna haja ya suala hilo kuangaziwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Masai alisema kuwa iwapo suala hilo litazingatiwa, basi itakuwa vyema kwa viwanda hivyo kukabiliana na moto kabla ya wazima moto kufika, huku akiishinikiza serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa magari ya wazima moto yanajazwa maji kila wakati.

“Kuna umuhimu mkubwa kwa viwanda vya mafuta na kemikali kuwa na vifaa maalum vya kudhibiti majanga hasa moto, kwani mara nyingi majanga hayo husababisha hasara kubwa na kuchangia vijana kukosa ajira kutokana na uharibifu wa mali,” alisema Masai.

Kiongozi huyo wa vijana alisema kuwa mikasa ya moto inayoshuhudiwa mara kwa mara imechangia katika kushuka kwa biashara pamoja na vijana wengi kufutwa kazi katika viwanda hivyo hali iliyochangia maisha kuwa magumu.

Mapendekezo ya Kiongozi huyo wa vijana yamejiri baada ya kiwanda cha mafuta na kemikali cha Solvochem eneo la Shimanzi mjini Mombasa kushika moto katika hali ya kutatanisha mwezi wa Januari.