Share news tips with us here at Hivisasa

Huku chanjo dhidi ya maradhi ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka tano ikitarajiwa kuanza siku ya Jumatatu, wazazi katika mtaa wa Kibera wamehimizwa kukumbatia huduma hiyo kwa kuhakikisha kuwa watoto wao wamepokea chanjo.

Kulingana na Justus Mwiti ambaye ni afisa wa afya katika kliniki ya Child and Family Wellness mtaani humo, ugonjwa wa polio unaweza kusababisha ulemavu kwa mtoto na hivyo kuna haja ya kuuzuia mapema.

"Wazazi wanastahili kuhakikisha kwamba watoto wao wenye umri wa chini ya miaka mitano wamepokea chanjo dhidi ya polio ili kuzuia uwezekano wao kupooza. Kwa kawaida, hakuna mzazi angependa mtoto wake awe na ulemavu, kwa hivyo ni vyema kukumbatia huduma hii kama suluhu," alisema Mwiti kwenye mahojiano na ripoti huyu katiuka kliniki hiyo.

Aidha, ameondoa hofu kwa wazazi wanao amini dhana kwamba chanjo dhidi ya polio ina madhara katika mwili wa mtoto.

"Kuna dhana kwamba chanjo hii si nzuri. Ningependa kuwaondolea wazazi wasiwasi kwa kusema kwamba dawa inayotumika katika huduma hii ni salama kwa afya ya mtoto,"alitoa hakikisho.