Share news tips with us here at Hivisasa

Wazazi mjini Mombasa wameunga mkono hatua ya Waziri wa Elimu nchini Dkt Fred Matiang’i ya kuubandua muungano wa wazazi, KNAPs unaoongozwa na Musau Ndunda.

Wazazi waliozungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumapili, walidai kuwa muungano huo hauna manufaa yoyote kwa wazazi licha ya wao kutakiwa kuuchangia kila mwaka.

Mmoja wao aliyetambulika kama Mr Wachira, aliutaja muungano huo kama ulioshindwa kuyatekeleza majukumu yake.

Alisema kuwa muubgani huo umefeli kuwatetea wazazi dhidi ya nyongeza ya karo ya mara kwa mara inayotekelezwa na baadhi ya walimu wakuu nchini.

“Kila shule zinapofunguliwa, wazazi tunalazimishwa kulipa kairo zaidi.Huo muungano wa wazazi mbona haujatutetea? Musau Nduda na wenzake waende nyumbani kabisa,” alisema Wachira.

Mapema wiki iliyopita, Waziri wa elimu Fred Matiangi aliwataka wazazi na shule kukoma kutoa mchango kwa muungano wa wazazi nchini Knaps, na kuutaja kama unaohudumu kinyume cha sheria za elimu kama ilivyonakiliwa mwaka 2013.

Kauli ya waziri huyo iliungwa mkono na mwenyekiti wa muungano wa walimu wakuu wa shule za upili KESSHA John Awiti, aliyeusuta muungano huo kwa kile alichokitaja kama kuwadhulumu walimu hao.

Hata hivyo, mwenyekiti Musau Ndunda, aliapa kumshtaki waziri wa elimu huku akidai kuwa muungano huo ni halali na unahudumu kwa mujibu wa sheria za elimu nchini.