Wazazi katika Shule ya msingi ya Majaoni, eneo la Shanzu, walitembelea afisi ya mkuu wa elimu katika eneo la Pwani, kulalamikia kuondolewa kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Wazazi hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw Steven Karanja, waliitaka idara ya elimu kumrejesha mwalimu huyo kazini huku wakipinga vikali madai kwamba nwalimu huyo ameshindwa kusimamia shule hiyo.
Akiongea wakati wa kikao hicho siku ya Jumatatu, Karanja alisema kuwa mwalimu mkuu huyo, Winston Mwatsama, amekuwa akifanya maendeleo shuleni humo na kuleta mabadiliko mengi.
“Tulishangazwa na hatua ya kusimamishwa kwa mwalimu huyo kwa madai ya kuendesha shule vibaya. Mbona wanamsumbua wakati sisi wenyewe kama wazazi hatujalalamika,” alisema Karanja.
Aidha, wazazi hao waliofanya kikao na mkurugenzi wa elimu katika eneo hilo la Pwani Bw Ibrahim Rugut walishtumu hatua ya mkuu huyo pamoja na waziri wa elimu nchini Fred Matiangi’ kuzuru shule hiyo kwa ghafla wakidai ilikuwa njama ya kumdhalilisha.
“Waziri Matiangi’ pamoja na Rugut walikuja shuleni kwetu ghafla. Madai kwamba mwalimu mkuu anatumia pesa vibaya ni uongo kwa sababu hata hajapewa pesa hizo,” alisema mzazi mmoja.
Hata hivyo, Rugut aliwaambia wazazi hao kwamba uchunguzi dhidi ya mwalimu huyo utaendeshwa na kwamba watatoa uamuzi kwa kipindi cha wiki tatu.
Waziri wa Elimu Fred Matiang’ pamoja na mkuu wa elimu katika eneo la Pwani Bw Ibrahim Rugut walizuru shule kadhaa katika eneo hilo na kuwataka walimu wakuu kueleza jinsi wanavyoendesha shule hizo.
Shule ya Majaoni ilikuwa moja kati ya shule zilizotembelewa na viongozi hao, ambapo mwalimu mkuu huyo anadaiwa kutumia vibaya pesa za kuendesha miradi shuleni.