Share news tips with us here at Hivisasa

Utawala kwenye kaunti ndogo ya Rongai jimbo la Nakuru, umetahadharisha wazazi kwamba oparesheni kali itafanywa hivi karibuni kwa lengo la kuwatia mbaroni wazazi wote wanaokosa kuwapeleka watoto wao shuleni, ama kuwatelekeza.

Akizungumza katika eneo la Kampi ya Moto mnamo Ijumaa, mkuu wa kaunti hiyo ndogo (DC) David Kosgei, alisema idadi ya watoto wanaozurura katika miji midogo ya kaunti hiyo ndogo imeongezeka maradufu.

“Tumepata vidokezo kwamba kuna wazazi ambao hawajali watoto wao kama wanaenda shuleni au la, kwa hivyo tutafanya oparesheni kukamata watoto hao, ambao watatuelekeza nyumbani mwao ili tuchukulie wazazi hatua,” akasema Kosgei.

Alisema kwamba badala ya vijana hao wa kati ya umri wa miaka 12-17 kuwa shuleni, wanaajiriwa na wanabiashara binafsi kama vijakazi wao.

“Pia hawa wanabiashara ambao wanawaajiri katika hoteli, maduka na nyumbani, tutawachukulia hatua kali za kisheria, kwa sababu kisheria mtu mzima ni ambaye amefikisha umri wa miaka 18 na ana kitambulisho cha serikali,” Kosgei aliongeza.

Aidha alitoa onyo kwa wenye vyumba vya burudani kama Video na michezo ya pool, wanaokubalia wanafunzi kuingia kwenye vyumba hivyo wakati wakitoka shule.