Wakazi wa eneo la Likoni mjini wameshauriwa kuwajibikia kikamilifu na kuwazuia watoto wao kuenda kesha za usiku.
Akiongea na wakazi wa Likoni siku ya Jumamosi, Mbunge wa Jomvu Badi Twalib alisema iwapo wazazi hao hawatajukumika vyema basi kesi za ubakazi na mimba za mapema zitaongezeka.
Alisema mara nyingi wazazi huwalaumu viongozi kwa kutowasadia kuwasilisha kesi hizo mahakamani kutokana na visa hivyo kuchangiwa na wazazi wenyewe na akiwasisitiza kuwalinda watoto wao.
“Tumeona mara nyingi wazazi wakitulaumu sisi viongozi kwamba hatuwasaidi kukabiliana na kesi za ubakaji na mimba za mapema lakini wazazi wenyewe ndio wanachangia na lazima wajukumike vyema," alisema Bw Badi.
Wakati huo huo, alisema kwamba Kaunti ya Mombasa kwa sasa inaongoza kwa visa vya ubakaji hasa watoto wa umri wa miaka chini ya 18.
Alisema kwamba zaidi ya watoto wanane kila siku hubakwa katika eneo la Likoni, Jomvu na Changamwe na akawasihi wazazi kuhakikisha kuwa wanawalinda watoto wao hasa wakike na kuwaripoti wahusika kwa maafisa wa polisi.