Afisa mkuu wa Idara ya Kilimo kwenye Kaunti ya Nakuru amewahimiza Wakenya na haswaa wazazi kuwajali watoto wote bila ya kuzingatia iwapo ni watoto wao au la.
Akizungumza kwenye eneo la Kikapu mjini Njoro siku ya Jumanne, kwenye ibaada ya misa ya wafu ya mmoja wa wavulana waliofariki kwenye ajali ya barabarani katika mkesha wa mwaka mpya katika eneo la Salgaa, Purity Muritu, alisema ni wajibu wa wazazi wote kuwashauri watoto.
Aliwataka wazazi kuwapa ushauri watoto ili kuhakikisha kwamba wanazingatia mienedo inayostahili.
Pamoja na hayo, amewataka watoto kutafuta ushauri wa wazazi wao kwa nyakati zote na pia kutowapuuza wazazi wao.
“Vijana wanapswa kuwaheshimu wazazi wao haswaa wanapowapa ushauri, kama njia moja ya kuboresha maisha yao ya siku za usoni,” alisema Muritu.
Aidha, amewahimiza vijana kuwasikiza wazazi wao haswaa wanapowapa ushauri kuhusiana na fedha, na kutilia maanani mawaidha wanayopewa.
Muritu alisema kuwa vijana kwa wakati mwingi husikiza ushauri wanaopewa kwa kutoa mfano wa mradi wa ukulima alioanzisha kwa husisha vijana, akisema vijana hao wamekumbatia miradi hiyo.
Wakati huo huo, alionyesha kusikitishwa kwake na idadi ya vijana wanaojihusisha na kilimo akisema idadi kubwa ya watu wanaojihusisha na kilimo kwa sasa ni wale walio na zaidi ya miaka 50.