Share news tips with us here at Hivisasa

Ili kuvikabili visa vya mimba za mapema miongoni mwa wasichana eneo la Pwani, ni lazima wazazi kujadiliana na watoto wao jinsi ya kuepukana na swala hilo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Afisa Mkuu wa Baraza Kuu la Kitaifa la idadi ya watu na Maendeleo eneo la Pwani Bi Margaret Mwaila alisema wasichana wadogo hujipata katika hali hiyo na lazima kuwaongoza watoto hao.

Kulingana na Bi Mwaila, wengi wa watoto wa kike hujipata katika njia panda baada ya kupachikwa mimba huku wazazi wao wakiwafurusha nyumbani licha ya wazazi hao kuchangia masaibu hayo.

Afisa huyo mkuu amewahimiza wazazi kujitahidi na kuwapatia watoto wao hususan wale wa kike mahitaji ya kimsingi ili kuwakinga na mimba za mapema.

“Ni lazima kwa wazazi kujitokeza kikamilifu na kuwaongoza watoto wao dhidi ya kujiepusha na mimba za mapema kwa kuwapatia mahitaji yote hasa wale wa kike kwani hatua hiyo itasadia," alisema Bi Mwaila.

Hata hivyo alidokeza kwamba swala hilo la mimba za mapema miongoni mwa wasichana limekuwa tatizo kubwa la kimaendeleo katika eneo la Pwani na linapaswa kutatuliwa kikamilifu.