Share news tips with us here at Hivisasa

Baraza la wazee wa kaya katika ukanda wa Pwani likiongozwa na Mwenyekiti wao Abdhalla Mnyenze, limetoa wito kwa viongozi kukamilisha ahadi zao walizoweka wakati wa kampeni ili kuafikia ajenda za kimaendeo.

Kwenye mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Mombasa, Mnyenze alisema kuwa asilimia sitini ya viongozi waliochaguliwa hawajatekeleza ahadi walizowaahidi wananchi.

Mnyenze alisema kuwa hatua hiyo imechangia kusambaratika kwa eneo la Pwani kimaendeleo, licha ya mfumo wa serikali za ugatuzi kutajwa kama suluhu itakayowaokoa Wakenya waliokuwa nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu.

Mnyenze alieleza kwamba kwa sasa baraza hilo linakagua utenda kazi wa viongozi hao.

Alisema kuwa wataungana kueneza sera za viongozi bora kwa wananchi, na kuwaelimisha kuhusu viongozi wanaostahili kuwachagua kwenye uchaguzi mkuu ujao, ili kubadilisha uongozi wa taifa.

“Sisi kama wazee wa kaya tutaungana na wananchi kuwashinikiza kuwachagua viongozi waadilifu, ili kubadili ongozi wa eneo la Pwani. Hakuna kiongozi aliyefanikisha agenda walizoahidi wakaazi wa Pwani,” alisema Mnyenze.

Wakati huo huo, mnyenze aliwatahadharisha wakaazi wa Pwani dhidi ya kupotoshwa na siasa za fedha, zinazotumiwa kama ngao kuu wakati wa kampeni.

Aliwataka badala yake kuunga mkono maono ya wazee ya kuweza kuwateua viongozi bora watakaojali maslahi ya wananchi na wala sio yao binafsi.