Kaunti ya Mombasa inalenga kutumia rasimali zake kuboresha sekta ya afya katika hatua inayolenga kuimarisha huduma za afya kwa wakaazi.
Akizungumza nje ya jengo la bunge la Mombasa siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge hilo, Mary Akinyi, alisema tayari serikali ya kaunti imeweka mikakati itakayo hakikisha kuwa zahanati na hospitali zinafanyiwa ukarabati.
Akinyi pia amelipongeza bunge hilo kwa kupitisha mswada wa afya bora, utakaoipa serikali ya kaunti uwezo wa kuongeza mgao wa fedha kwa sekta ya afya katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao.
Mswada huo aidha utaiwezesha serikali ya kaunti kutumia pesa kununua vifaa vipya na pia kununua dawa ili kulikabili tatizo la uhaba wa dawa, ambalo wakati mwingine hukumba baadhi ya hospitali za kaunti hiyo.
Hatua hii huenda ikaleta afueni kwa wakaazi ambao mara nyingi hulalamikia huduma mbovu inayotolewa katika baadhi ya hospitali mjini humo, ikiwemo ukosefu wa dawa katika hospitali ya Mkoa wa Mombasa.