Shirika la kiserikali la SCOPE limesema kuwa limefanikiwa kuwanusuru zaidi ya watoto 100 kuotka biashara ya ukahaba katika eneo la Pwani.
Akiongea na waandishi wa habari Jumanne mjini Ukunda, afisa msimamizi wa shirika hilo Emmanuel Kahaso alisema kuwa wanaendeleza kampeni hizo wakilenga maeneo ya Ukunda, Msambweni na Lungalunga na maeneo mengine katika eneo hilo.
“Tunalenga watoto wenye miaka saba hadi 12, na tunawarudisha shuleni kwa sababu hawa watoto wanataka kuendelea na maisha yao lakini umaskini unawafanya wanachukua fursa ya utalii eneo hili na kuingia katika hii biashara haramu,” alisema Kahaso.
Shirika hilo lililo chini ya ufadhili wa hifadhi ya watoto ya Terre des Homes linailaumu jamii kwa kuchangia pakubwa katika ongezeko la watoto wanaoingia katika biashara hiyo kwa kutozingatia majukumu yao.
Licha ya kwamba eneo la Ukunda lina sifa ya utalii katika ukanda wa Pwani, zaidi ya watoto 400 wanakisiwa kuhusika katika biashara ya ngono eneo hilo jambo linalotia hofu kuhusu kizazi kijacho.